AJIRA ya kwanza ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Joseph Magufuli (55) ilikuwa ni ualimu na atasherehekea siku yake ya kuzaliwa siku nne tu baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwa
mujibu wa wasifu wake uliogawiwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM
uliomchagua kuwa mgombea juzi katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM uliopo
Dodoma, Magufuli alianza kazi akiwa mwalimu wa masomo ya kemia na
hisabati katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Mwanza
Kwa
maana hiyo, mgombea urais huyu ni mwanasayansi na kama atachaguliwa
kuwa Rais wa Tano wa Tanzania kwa kuwashinda wagombea wa upinzania, basi
atakuwa Rais wa kwanza mwanasayansi kuitawala Tanzania.
Marais
waliomtangulia; Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan
Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete ni wasomi katika fani ya ama
sanaa au uchumi, hakuna mwanasayansi.
Magufuli
alizaliwa Oktoba 29, 1959 katika Wilaya ya Chato ambayo ni mojawapo ya
wilaya tano za mkoa mpya wa Geita uliopo kaskazini magharibi mwa
Tanzania.
Wilaya ya Chato ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na ni mwaka 2012 tu ndipo ilipohamishiwa Mkoa wa Geita.
Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Chato ina jumla ya
wakazi 365, 127; huku wengi wao wakiwa na asili ya kabila la Wasukuma.
Magufuli
alipata elimu ya msingi katika Shule ya Chato na masomo ya sekondari ya
awali katika Seminari ya Katoke, Biharamulo. Alimalizia kidato cha nne
katika Shule ya Sekondari Lake, mkoani Mwanza. Kidato cha sita
alimalizia katika sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa.
Wasifu
wa Magufuli unaonyesha kwamba alipata cheti cha Stashahada ya Ualimu
katika Chuo cha Elimu Mkwawa mnamo mwaka 1982 – alikojikita zaidi katika
masomo ya hisabati na kemia
Kati
ya mwaka 1985 hadi 1988, Magufuli alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kwa ajili ya masomo yake ya shahada ya kwanza ya ualimu wa kemia
na hisabati.
Waziri
huyo wa Ujenzi alijipatia shahada yake ya uzamili kwenye kemia kupitia
Vyuo Vikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Salford cha Uingereza kati ya
mwaka 1991 na 1994.
Wakati
akiwa waziri katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009, Magufuli
alijiunga na UDSM alikosomea Shahada ya Uzamivu katika kemia
(PhD-Chemistry).
Magufuli
aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza mwaka 1995 wakati
alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, na
hajawahi kukaa nje ya baraza hilo tangu wakati huo
Amewahi
kuwa waziri katika wizara tofauti kama vile Wizara ya Ujenzi, Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Mwanasiasa
huyu ni mwanataaluma mbobezi, akiwa tayari ni mwanachama wa vyama vya
kitaaluma kama Chama cha Wakemia wa Tanzania na kile cha Wataalamu wa
Hisabati Tanzania.
John
Joseph Pombe Magufuli ana mahaba na namba. Si kwamba amesoma hisabati
kama somo lakini amekuwa akipenda masuala ya namba na moja ya alama yake
kubwa ya kiutendaji ni uwezo wake mkubwa wa kukariri takwimu mbalimbali
kuhusu masuala anayoyafanyia kazi.
Kama
msomi, Dk. Magufuli ameandika machapisho mbalimbali yakiwamo; “A New
Rate Equation for Solid State Decomposition and its Application to the
Decomposition of Calcium Carbon Trioxide, The Control and Management of
Heat as Challenge and Opportunity to Engineers, Funding for the EAC Road
Network Project na The Potential of Anacardic Acid Self-Assembled
Monolayer From Cashew Nut Shell Liquid As Corrosion Protection Coating
(2009).
Mke wa Magufuli, Janet, ni Mwalimu wa Shule ya Msingii Mbuyuni, shule aliyokuwa akifundisha Salma, mke wa Rais Jakaya Kikwete.
Sifa nyingine ya ziada ya John Pombe Magufuli ni kwamba hanywi pombe wala havuti sigara