Hii tamaa ya wafanyabiashara, ambayo haijali hata afya na maisha ya wateja wao inasikitisha sana. Baadhi ya kampuni zinazouza kuku, kama hii iliyonaswa kwenye video, zimestukiwa kuwa zinawajaza kuku wembamba ili kuwanenepesha na kuwaongeza uzito kabla ya kuwauza, kwa kutumia kimojawapo au mchanganyiko wa yafuatayo:
- Maji ya chumvi
- Kemikali za kuongeza ladha, na za kulainisha. Sababu kuku hao wamekuzwa haraka na kwa madawa, huwa hawana ladha ya asili
- Vimiminika/mabaki ya ng’ombe na nguruwe kutoka machinjoni
- Mwani au “seaweed” (mimea/magugu ya baharini)
Ukiachilia mbali utapeli kwa wateja, uchakachuaji huu pia unahatarisha afya zao, na kudhulumu haki zao za kidini, kama mamilioni ya Waislam, na Wayahudi nchini Uingereza wanaokula kuku bila kujua kuwa kuku hao wameshindiliwa mabaki ya nguruwe (soma: Chicken injected with beef and pork waste sold in UK.) katika mchakachuo huu unaoitwa “chiken plumping”(nenepesha kuku,) kuku hao huongezwa takriban asilimia 30 ya uzito wao wa awali; karibia theluthi nzima. Video chini inaonyesha mojawapo ya mbinu na kifaa vinavyotumika katika uchakachuaji huo
Mojawapo ya dalili inayoonyesha kuwa kuku amechakachuliwa, ni kusinyaa kwa kiasi kikubwa anapopikwa. Kwa muda baadhi ya wateja wa nchi mbalimbali za Ulaya na Asia walikuwa wanashangaa wanaponunua kuku mkubwa aliyenona, lakini mara baada ya kupikwa, wanasinyaa kuliko kawaida.
Kwenye video hapa chini, huyu jamaa anaonjesha ni kiasi gani nyama ya kuku aliyonunua ilivyochakachuliwa. Aliweka nyama hiyo ya kifua cha kuku kwenye kikaango, bila mafuta wala maji, na kukipika kwa moto wa chini, na sasa analakamika na kuonyesha maji kibao yaliyotoka ndani ya nyama hiyo. Anasema ni Ulaya kusini, na Africa tu ambako amewahi kula kuku wazuri wa asili, na watamu. Lakini kuku wa Ulaya ya juu, USA, na Asia wanachakachuliwa zaidi