MWANAMUME
yeyote anapotaka kumtongoza mwanamke hulazimika kwanza kumwonesha –
japo kwa matendo – kuwa anampenda, au kwamba amevutiwa naye, hata kama
ni kimwili tu. Hatua hii ndiyo yenye changamoto kubwa zaidi kwa
mwanamume, maana ndipo wakati anapokuwa anajaribu kufikisha ujumbe kwa
mlengwa huku yeye mwenyewe akijihakikishia kuwa haharibu mambo.
Mwanamume anapokuwa
anajaribu kufikisha ujumbe wa “nakupenda” kwa mwanamke, mapigo ya moyo
yanaweza kumwenda mbio, hususan kama mwanamke mwenyewe anaonekana kuwa
“maji marefu”. Hata hivyo, ni kazi ambayo kila mwanamume hulazimika
kuifanya.
Kazi hii ya kufikisha
ujumbe kwa mara ya kwanza huhitaji umakini. Bahati njema, shughuli
yenyewe ina sayansi yake, ambayo ina misingi katika mahusiano ya
kijamii. Ukifahamu sayansi hii inaweza kuwa rahisi zaidi kwako kufikisha
ujumbe kwa mtarajiwa wako – na kufanikiwa.
1. KUKUTANISHA MACHO NI MUHIMU
Kawaida, mambo yote
huanzia – na pengine kuishia – katika kukutanisha macho. Mwanamke
atakapobaini kuwa hujajaribu kumwangalia japo kwa sekunde mbili
mfululizo, ataondoa mawazo na hisia zake kwako hata kabla hujasema neno
lolote.
Macho ndizo zana muhimu
zaidi mtu anapokuwa anataka kufikisha ujumbe kwa mwenzake kuwa
anampenda, au amevutiwa naye. Hii ni kwa sababu macho ndiyo vipitisho na
visambazaji muhimu vya ishara baina ya mtu na mtu, hata kama si katika
masuala yanayohusiana na mapenzi.
Kukutanisha macho na mtu
wa jinsia nyingine unayevutiwa naye au anayevutiwa nawe ni jambo lenye
nguvu za ajabu katika kuanzisha uhusiano. Kwa sababu hiyo, hata
unapofanikiwa kumtazama moja kwa moja machoni mwenzako hutarajiwi
kutumia zaidi ya sekunde mbili, kutokana na nguvu iliyomo katika
mawasiliano haya.
Katika hili, wanaume
mahiri hufahamu ni wakati gani wa kumwangalia mwanamke na ni wakati gani
wa kutomwangalia. Mara nyingi, ni vizuri zaidi kumwangalia zaidi
mwanamke wakati anapozungumza, huku ukikwepesha macho kidogo pale
unapozungumza wewe.
2. UNATAKIWA UWIANO, UKWELI KATIKA MAZUNGUMZO
Ni jambo lisilopingika
kwamba wanaume na wanawake wanatofautiana katika maana ya dhana ya
mawasiliano. Hata hivyo, bado inawezekana kuendesha mazungumzo
shirikishi na yenye kuburudisha ukiwa na mwanamke, bila kuonekana wa
bandia.
Watu wa jinsia zote mbili
wanaweza kutuhumiwa kwa kupindisha ukweli na kujaribu kuficha tabia na
mienendo yao wanapozungumza na wapenzi watarajiwa. Naam, katika
mazungumzo ya kwanza baina ya wapenzi au wachumba watarajiwa uwongo –
ukiwemo ule usiotarajiwa – huwa mwingi.
Katika mazungumzo ya
kwanza ni kawaida kwa mwanamume kubadilisha matendo yake na mtindo wake
wa kuzungumza kwa maslahi ya kumpata mwanamke, jambo ambalo huifanya
hulka yake ya wakati huo kuwa ya bandia. Lakini pia wasichana/wanawake
husema “Nakupenda” bila kumaanisha, pengine kwa ajili ya kumfurahisha
mwanamume, au kusikia mwanamume atasemaje.
Jambo la muhimu katika
mazungumzo ya awali baina ya mwanamume na mwanamke ni kuepuka michezo ya
kudanganyana na kukwepana, badala yake, yafanye mazungumzo kuwa rahisi
na halisi. Hapo ndipo mwanamume hujitofautisha na wanaume wengine na
kupendwa kwa sababu hiyo.
3. USIPUUZE NGUVU YA LUGHA YA MATENDO
Wakati mtu anapokuwa
akijaribu kuwasilisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa mwenzake, lugha ya
matendo yake huzungumza kwa sauti kubwa zaidi kuliko maneno yake. Hili
limeweza kuthibitishwa kwa nyakati mbalimbali kutokana na tafiti
mbalimbali.
Katika muktadha wa
kujaribu kufikisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa mlengwa, lugha ya matendo
ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi. Kwa hakika, asilimia kubwa ya ujumbe
unaowasilishwa kwa mlengwa huwasilishwa kwa njia ya matendo ya mwili na
si maneno.
Ni asilimia ndogo tu ya ujumbe inayowasilishwa kwa maneno –
na wakati mwingine maneno huweza kuleta matatizo maana katika kuzungumza
kuna kujikwaa kwingi, kwani ulimi hauna mfupa.
Ili uweze kufanikiwa
katika kueleza nia yako kwa mwanamke, lazima ujue jinsi ya kutumia lugha
ya matendo yako. Na pengine hutatumia nguvu, maana watu husema penzi
kikohozi – kama unalo litaonekana tu machoni pa mlengwa.
Ukitafakari kwa makini
utabaini kuwa huhitaji kusema sana ndipo uweze kupendwa, kwani maneno
huchangia asilimia kidogo tu. La muhimu ni kuhakikisha kuwa mlengwa wako
anakusoma na kukuelewa vizuri kwa kuangalia matendo ya mwili wako.
4. ACHA ASILI ICHUKUE MKONDO WAKE
Katika nadharia
mbalimbali za kijamii na kidini ni jambo la kawaida kusikia kuwa
binadamu wote ni sawa. Hata hivyo, katika muktadha wa kimapenzi, kila
mtu mmoja mmoja anafahamu kabisa kuwa si kila mwanamume/mwanamke ni sawa
na mwenzake.
Methali yenye asili ya
kimagharibi husema “Uzuri wa mtu uko katika macho ya yule anayemtazama.”
Hii ina maana pia kwamba, kila mtu anavyo vigezo vyake vya uzuri kwa
kuzingatia maumbile yake. Pia jamii zinavyo vigezo vya uzuri, lakini
hutangulia kwanza vigezo binafsi.
Unapokuwa umekaa na
mwanamke ambaye anakuvutia kwa mwonekano wake, sauti yake na kadhalika,
si rahisi sana kujizuia kuonesha kuwa anakuvutia. Hii ni kwa sababu si
wewe, bali ni nafsi yako inayokusukuma. Na yeye mwenyewe atakusoma kwa
kuangalia lugha ya matendo yako na kukwelewa, utakaobaki ni uamuzi wake
tu.
Katika jamii kuna vigezo
kuhusiana na kiuno, miguu, maziwa, makalio na kadhalika. Wengi wa
wanajamii huvizingatia na kuongeza vyao. Huu ni ukweli wa kibiolojia
ambao hauwezi kupingika.
Mwanamke mwenye vigezo vinavyokubalika zaidi
katika jamii yake atawavutia wanaume wengi zaidi. Hapa mwanamume
hahitaji kutumia nguvu nyingi – asili ya maumbile itamsaidia
humtambulisha mwanamke kuwa amempenda.
5. TUMIA CHANGAMOTO YA WALAKINI
Mara nyingi changamoto
kubwa katika suala zima la mtu kubainisha nia yake kwa mwanamke hutokana
na ukweli kwamba katika mchakato mzima huwa kuna wasiwasi na walakini.
Kwa hakika, jambo hili ni la “pengine” au “labda” kutokana na kutoweza
kufahamu kirahisi mwenzako anawaza nini.
Unapoonesha nia yako ya
kumpenda mwanamke, ni kama unaamsha hisia zake kwako na ni kama vile
unamuuliza: “Ungependa kuwa nami?” Kwa njia hii ni kama utakuwa
unafungua mlango wa kupata jibu la “ndiyo” au “hapana” kwani huyo
unayemwonesha kuwa unampenda na yeye ana matakwa yake na mapendeleo
yake.
Kimsingi hakuna kanuni
wala sheria rasmi unazopaswa kuzingatia wakati wote. La muhimu ni wewe
mwenyewe kujiachia na kuingia katika maji usiyofahamu kina wala mwisho
wake, bali wewe nenda na mkondo wake huku ukitarajia kuwa lolote
linaweza kutokea. Hiyo ndiyo sehemu ya raha yake.
6. DHIBITI HISIA, MIHEMKO
Tofauti na mwanamke,
mwanamume anayejaribu kuonesha nia yake hatakiwi kujiweka katika mkao wa
mwanamitindo.
Wanawake ndio hufahamika zaidi kwa mikao yao “ya kula”
wanapokuwa katika mawindo (japo wengi hubisha), lakini si mwanamume.
Wanawake ndio hutarajiwa kujieleza zaidi kwa njia ya matendo na mikao,
lakini wanaume hutarajiwa kudhibiti hisia na mihemko yao .
Tofauti katika lugha ya
matendo baina ya watu wa jinsia mbili hutokana na maumbile ya kujenetiki
pamoja na utamaduni wa jamii husika.
Yote yakizingatiwa, matakwa ya
mwanamke ndiyo hupewa kipaumbele zaidi. Kwa ufupi, matendo ya kutongoza
ya mwanamke huwa wazi zaidi, lakini mwanamume hulazimika kuficha hisia
na mihemko yake.
Wajibu wa kufikisha
ujumbe kwa mtu wa jinsia tofauti ni wa kila mmoja – mwanamume na
mwanamke.
Hata hivyo, wanaume ndio wenye jukumu kubwa zaidi la
kuanzisha, kwa kuzingatia utamaduni wa jamii nyingi. Unaweza ukaona
ugumu, lakini ipo sayansi itakayokusaidia. Kama una wasiwasi na uwezo
wako, ni vizuri kuyazingatia yote yaliyobainishwa hapa.